Nguvu ya Umoja: Jinsi “WikiGap 2026” Inavyopindua Meza katika Wikamusi ya Kiswahili

Translate this post

Katika ulimwengu wa maarifa huru, takwimu hutoa picha, lakini ushirikiano ndio hutoa uhai. Kati ya Januari na Mei 2026, kikundi cha Jenga Wikipedia ya Kiswahili (JWK) kiliingia mtaani kikiwa na dhamira moja: kutumia kampeni ya kimataifa ya WikiGap si tu kuziba pengo la kijinsia, bali kuleta mapinduzi ya kidijitali katika mradi wa Wiktionary (Wikamusi) ya Kiswahili.

Lengo letu lilikuwa bayana: kuivuta Wikamusi ya Kiswahili ifikie rekodi ya kihistoria ya ingizo 80,000. Hivi ndivyo tulivyoweza kugeuza ndoto hiyo kuwa uhalisia kupitia awamu mbili za kipekee na ushirikiano madhubuti wa kijumuiya.

Picha ya pamja siku ya warsha mnamo tar. 11 April, 2026 katika Maktaba Mpya ya UDSM

Awamu ya Kwanza: Kupigilia Misumari ya Msingi

Awamu ya kwanza ya kampeni yetu (Januari 6 – Machi 31) ilikuwa ni kipimo cha uvumilivu. Tulijikita katika orodha maalum ya makala za Wikipedia, huku tukiendelea kusukuma maneno kwa wingi kwenye Wikamusi.

Kulingana na Dashibodi yetu ya Awamu ya Kwanza, matokeo yalikuwa ya kishindo:

  • Makala Mapya 17,000 (Jumla ya miradi yote)
  • Haririo 23,400
  • Wasomaji 157,000 walioona kazi zetu.

Wakati Wikipedia ikikua kwa makala mpya 1,460, mradi wa Wikamusi uling’ara zaidi kwa kupata ingizo mpya 15,600. Awamu hii ilituthibitishia kuwa injini yetu ya ndani ilikuwa na nguvu, lakini ili kufikia lengo la 80K, tulihitaji kupanua wigo.

Awamu ya Pili: Warsha ya “Umoja ni Nguvu”

Kampeni ilishika kasi mpya mnamo Aprili 11, 2026, ndani ya Maktaba Mpya ya UDSM (Chumba namba 221). Hii haikuwa warsha ya kawaida; ilikuwa ni muunganiko wa nguvu kati ya JWK na Jumuia ya Wikimedians of Arusha.

Mbegu ya ushirikiano huu ilipandwa kule Zanzibar wakati wa National Retreat mwishoni mwa mwezi Machi. Eben, kiongozi wa jumuia ya Arusha, alionyesha shauku kubwa ya timu yake kujifunza ufundi wa ndani wa Wikamusi. Hatukusita. Chini ya uongozi wa Madam Aneth David na sapoti kubwa kutoka kwa Anuary Rajabu (Wikimedia Tabora), tulifanya kikao cha pamoja (joint session) kilichoziba pengo la kijiografia na kiufundi.

Matokeo ya umoja huu yameandikwa kwenye Dashibodi ya Awamu ya Pili:

  • Idadi ya Wahariri: Iliongezeka kutoka 16 hadi 45.
  • Ukuaji wa Wikamusi: Makala mpya 7,940 ndani ya mwezi mmoja pekee.
  • Midia: Picha 124 zilipakiwa Wikimedia Commons, zikiongeza uhai wa picha katika harakati zetu.

Kwa Nini Hili ni Muhimu?

Tangu mwaka 2024, Jenga Wikipedia ya Kiswahili imekuwa ndiyo affiliate pekee nchini inayowekeza nguvu kubwa kwenye Wikamusi. Kuona Jumuia ya Arusha ikiungana nasi katika mapambano haya ya kitaalamu ilikuwa ni jambo la faraja kubwa.

Tulipotenganisha takwimu, tuliona jambo la kufurahisha: wakati kundi dogo likiendelea na Wikipedia (makala mpya 135 katika awamu ya pili), “shambulio” kubwa la wahariri 22 lilielekezwa Wikamusi. Hii ilituzalishia zaidi ya maneno 356,000 mapya kwa mwezi wa Aprili pekee.

Hitimisho

Robo hii ya tatu ya mwaka 2026 imethibitisha kuwa harakati za Kiswahili sasa si za mtu mmoja mmoja tena; ni za ushirikiano wa kimkakati. Tunapoelekea kufikia lengo letu la ingizo 80,000, tunabeba somo moja kuu: Umoja ni Nguvu.

Tunapobadilishana ujuzi kati ya Arusha, Tabora, na Dar es Salaam, lugha ya Kiswahili haibaki tu hai mtandaoni—bali inatawala. Tazama shajara ya maendeleo yetu hapa: Wiktionary:Matukio ya hivi karibuni – Wiktionary

Can you help us translate this article?

In order for this article to reach as many people as possible we would like your help. Can you translate this article to get the message out?

Notify of
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments