Tangazo la Maeneo ya Wikimania 2025 na 2026

Translate this post

22 September 2023 by Mehrdad Pourzaki

Translate This Post

Wikimania ni fursa adimu kwa wachangiaji wa Wikimedia kutoka kote ulimwenguni kukusanyika pamoja ili kusherehekea, kushirikishana, kuungana na kukua. Wikimania 2023 – iwe tulishiriki mtandaoni au ana kwa ana – ilikuwa ni ukumbusho mzuri wa jambo hili na mengine mengi. Mkutano wa Wikimania 2023 pia ulifanya majaribio ya muundo wa ushirikiano wa kikanda ukihusisha timu kuu ya waandaaji wa kujitolea na umeleta matokeo mazuri sana. Kama vile Kamati ya Uongozi ya Wikimania ilivyokuwa imetarajia, tulishuhudia faida ya kuwa na waandaaji wa hapo baadaye kushiriki na kujifunza kutoka kwa waandaaji wa sasa, kama vile timu za 2023 ESEAP na 2024  CEE.

Kwa ari hiihii, tunatangaza waandaaji wa Wikimania kwa mwaka 2025 na 2026.

Twiga akiwa na madhari nzuri nyuma yake ya jiji la Nairobi City Skyline , Alexmbogo, CC BY-SA 4.0

Jambo Afrika Mashariki!

Chimbuko la historia, bioanuwai, sanaa na usanifu, na kitovu cha ushirikiano baina ya serikali, teknolojia, na mengine mengi, Afrika Mashariki imejaa fursa lukuki kwa Wikimedia. Wikimania 2025 itaandaliwa kwa ushirikiano wa aina mbalimbali wa wachangiaji  wa kujitolea na washirika wa Wikimedia waliopo Afrika Mashariki. Tulifurahi kupokea nia mbalimbali kutoka kwa Wanawikimedia kutoka kwenye kanda hii kushirikiana na kukaribisha Wikimania. Huu utakuwa ni mkutano wa Wikimania wa 20 na hatua muhimu kama mkutano wa Wikimania wa tatu barani Afrika, wa pili pekee barani Afrika kusini mwa jangwa la Sahara, na wa kwanza kwa ukanda wa Afrika Mashariki. Tunaamini katika tija ya mkutano huu wa Wikimania katika kuzitia nguvu zaidi jumuiya mpya na zilizo hai  katika kanda hii na kukuza ukuaji wa maudhui na michango ambapo kwa sasa tuna mapungufu makubwa. Pia mkutano huu wa Wikimania utaleta fursa mpya ya kusherehekea mafanikio ya Wanawikimedia katika kanda hii na katika bara zima la Afrika. Jiji ambalo litakuwa mwenyeji wa mkutano wa Wikimania litaamuliwa ndani ya miezi ijayo kulingana na tathmini za kisiasa na usalama, pamoja na maoni kutoka kwa waandaaji wazoefu, wadau wa Wikimedia, na washirika wa ndani.

Jambo Paris!

Mkutano wa Wikimania wa 2026 utaandaliwa mjini Paris na Wikimedia Ufaransa kwa kushirikiana na WikiFranca, chama cha kimataifa kinachowaleta pamoja watu binafsi na vikundi vya watu wanaozungumza lugha ya Kifaransa katika harakati za Wikimedia. Huu utakuwa ni mkutano wa Wikimania wa kwanza kufanyika nchini Ufaransa na wa kwanza kwa kushirikiana kimataifa na jumuiya zinazozungumza Kifaransa. Paris itakuwa mazingira mazuri kwa mkutano huu maalumu wa Wikimania unaoadhimisha kumbukumbu ya miaka 25 ya matoleo mengi ya Wikipedia, kama vile Kibasque, Kikatalani, Kifaransa, Kijerumani, Kiitaliano, Kireno, Kihispania, Kiswidi na zinginezo, ikiwa ni pamoja na Kiingereza. Kuanzia ukingo wa Seine hadi vilele vya vilima na minara, kutoka makumbusho za kimataifa hadi maktaba na mikahawa ya kihistoria ambamo wanafalsafa waliwahi kubishana, tutakuletea miaka 25 ijayo ya maudhui ya wazi na ushirikiano wa maarifa ya bure tutakapokutana pamoja mwaka 2026 kusherehekea hatua hii kuu huko Paris … au mtandaoni – ili kusherehekea hatua hii kubwa.

Kamati ya Uongozi ya Wikimania inafuraha kutoa tangazo hili kwa ushirikiano na Shirika la Wikimedia Foundation, Kitovu cha Kikanda na Kimada cha Afrika Mashariki (EARTH), Kamati ya Uendeshaji ya Wiki Indaba (WISCom), WikiFranca, na Wikimedia Ufaransa.

Katika ua ya Makumbusho ya Louvre ukiwa unaangalia magharibi, Benh LIEU SONG, CC BY-SA 4.0

Wikimania 2024 na 2027

Wikimania inaundwa kwa ushirikiano na Wanawikimedia kutoka kote ulimwenguni. Iwe wewe ni mhariri mwenye uzoefu, mgeni ambaye umejiunga na harakati katika mkutano wa Wikimania, mtetezi mwenye shauku ya maarifa ya wazi, au mwandaaji matukio mwenye shauku, Wikimania ni nafasi ya kuunda mfumo ikolojia wa harakati zetu. Wikimania 2024 itafanyikia Kraków, Poland – maandalizi tayari yanaendelea na wito wa watu wa kujitolea utazinduliwa hivi karibuni. Tafadhali shiriki katika majadiliano ya kwenye wiki, changia kwenye kipindi iwe ana kwa ana au mtandaoni, au jiunge na kamati ndogondogo ili kusaidia timu zinazoandaa. Kuna kitu kwaajili ya kila mtu katika Wikimania. Kushiriki katika matukio kumebadilika sana katika miaka michache iliyopita na ni lazima tuendelee kuboresha ushiriki wa mseto na kupitia mtandaoni na kupanua maudhui yanayohitajika kwa saa zote za eneo.

Kuchagua maeneo miaka kadhaa kabla kunamaanisha kupunguza shinikizo kwa waandaaji na kupata chaguo bora zaidi la maeneo, muda zaidi wa michakato ya visa, na fursa kubwa zaidi za kujifunza na kushirikiana. Kwa Wikimania 2027, tunatumai kutoa wito wa kutuma nia mwaka ujao, hasa kukaribisha nia kutoka maeneo ambayo hatujafika kwa muda mrefu, kama vile Amerika ya Kusini, au yale ambayo bado hatujayapelekea Wikimania, kama vile Asia Kusini.

Kamati ya Uongozi ya Wikimania – inakaribisha wanachama wapya

Harakati za Wikimedia ni alama ya mwanga wa msukumo, jukwaa la uvumbuzi, na sherehe ya ushirikiano baina ya binadamu, na Wikimania ni mkutano wake wa kila mwaka. Imeandaliwa na watu wa kujitolea na kuratibiwa na Shirika la Wikimedia Foundation, Wikimania ni sherehe ya utofauti wa watu wetu na michango. Inaangazia uwanda mpana wa programu, ikijumuisha mazungumzo, warsha, hackathons, na bila shaka, matukio ya kijamii. Wikimania ina fursa kubwa kwa tija za ndani- iwe ni kwa kukaribisha wageni ama kuwapa nguvu zaidi wachangiaji waliopo, au kwa miji mwenyeji, nchi mbalimbali na maeneo ambayo kiasili maudhui yanaboreka na kupanuka zaidi pale ambapo Wanawikimedia wamepata nafasi ya kuchunguza – Wikimania  2023 ni mfano bora wa hii.

Kama wasimamizi wa Wikimania, Kamati ya Uongozi huweka uangalifu mkubwa na mazingatio katika kuchagua maeneo ya kufanyia mkutano. Hii ni pamoja na fursa zenye tija, uwezekano wa ukuaji wa harakati, urahisi wa kusafiri, usalama, upatikanaji wa visa, kumbi, vifaa, na zaidi. Hakuna eneo kamilifu. Ndiyo maana katika kufanya uamuzi wetu, tunashauriana na Shirika la Wikimedia Foundation, timu za waandaaji za jumuiya na wataalamu wa matukio. Tafadhali tujulishe kama ungependa kujiunga na mazungumzo haya. Pia tunatafuta wanajumuiya wapya walio na uzoefu wa kuandaa Wikimania au matukio mengine ili kujiunga na Kamati ya Uongozi. Tafadhali wasiliana nasi kwenye wiki au kupitia wikimania@wikimedia.org.

Picha ya pamoja ya Wikimania 2023, ZMcCune (WMF), CC BY-SA 4.0

Can you help us translate this article?

In order for this article to reach as many people as possible we would like your help. Can you translate this article to get the message out?

No comments

Comments are closed automatically after 21 days.